Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi imepata mali iliyopatikana kwa njia isiyo halali yenye thamani ya shilingi bilioni 3.4 katika mwaka wa kifedha wa 2024/2025, kutoka Ksh 2.9 bilioni zilizopatikana mwaka uliopita.
Wakati wakizindua ripoti hiyo ya kila mwaka, mwenyekiti wa EACC David Oginde na Afisa Mkuu Mtendaji Abdi Mohamud, hata hivyo, walikashifu utekelezwaji hafifu wa sura ya sita ya katiba wakitaja kuingiliwa na mashahidi kuwa tatizo kuu katika vita dhidi ya ufisadi.
Kadhalika ripoti hiyo imeonyesha kuwa rushwa ilibaki kuwa kosa lililoripotiwa zaidi nchini. Masuala ya ufujaji wa fedha, mwenendo usio wa kimaadili na ununuzi wenye udanganyifu yaliorodheshwa kama masuala yaliyoripotiwa na kuchunguzwa na tume. EACC pia imesikitishwa na kuongezeka kwa idadi ya maafisa wa serikali na umma ambao hutumia vyeti bandia za kitaaluma kupata ajira.
Kaunti na mashirika ya umma ni miongoni mwa mashirika yanayochunguzwa kwa ubadhirifu wa hazina ya umma.