Katika hatua za kuimarisha amani kaunti ya Pokot Magharibi Gavana wa kaunti hii Simon Kachapin ameongoza makabidhiano ya pikipiki 120 kwa makasisi wanaohusika katika uenezaji amani katika eneo la Pokot Magharibi na kaunti jirani. Pikipiki hizo zitaongeza uwezo wa wachungaji wanaofanya kazi katika maeneo ya mipakani ambapo amani bado ni changamoto.
Aidha Kachapin amesema msaada huo unafuatia ahadi iliyotolewa na Rais William Ruto wakati wa maombi ya madhehebu mbalimbali huko Chesombur na umefanikishwa kupitia Ushirikiano wa Maaskofu wa kaunti ya Pokot Magharibi.

Makanisa 43 kila moja yalipokea pikipiki, huku mgao wa ziada ukitolewa kwa kaunti za Marakwet na Baringo, ambazo zilipokea pikipiki 25 kila moja, Turkana 20, na Samburu tano.
Kadhalika gavana huyo ameongeza kuwa viongozi wa kidini wanasalia kuwa washirika wakuu katika kukuza amani, utangamano na kuishi pamoja, na mpango huu unaonyesha ushirikiano unaoendelea kati ya serikali ya kitaifa na serikali za kaunti katika kuimarisha juhudi za mashinani za kujenga amani.