Waziri wa Kilimo Mutahi Kagwe amesema kwamba serikali italipa malipo yote ambayo hayajalipwa kwa wafanyakazi katika viwanda vya sukari nchini.

Akizungumza wakati wa mkutano na Muungano wa Wafanyakazi wa Sukari na Bodi ya Sukari ya Kenya Pamoja na wawakilishi wa viwanda vinne vya sukari vilivyokodishwa, Waziri huyo amesisitiza kwamba kulipa madeni ya wafanyakazi bado ni kipaumbele kwa utawala.

Waziri Kagwe amebainisha kwamba mpango wa malipo tayari unaendelea, akiongeza kwamba serikali pia imeanza kulipa ada za muda mrefu zinazodaiwa wakulima wa miwa.

Aidha Waziri Kagwe amesisitiza kwamba serikali imejitolea kufufua sekta ya sukari, akisema kwamba ukodishaji wa viwanda muhimu vinavyomilikiwa na serikali unaashiria mabadiliko ya kimkakati kuelekea uendelevu, ufanisi, na kubuniwa kwa nafasi za ajira.