Watu watano, wakiwemo maafisa wakuu wa kliniki ya kibinafsi huko Oyugis na wafanyakazi kutoka Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), wamefikishwa mahakamani kwa madai ya kula njama ya kuilaghai Mamlaka hiyo zaidi ya Ksh. milioni 17.5 kupitia madai ya kimatibabu yaliyoghushiwa.

Washtakiwa hao, Arthur Otula, Rosemary Daraja, Peter Abuna, Robert Ingasira, na Archprime Medical Clinic Oyugis Ltd walifika mbele ya mahakama ya Nairobi ambapo walikana mashtaka kumi kuanzia kula njama hadi kudanganya, kudanganya taarifa za afya, kupata na kutumia mapato ya uhalifu, hadi kutoa hati za uongo na matumizi mabaya ya fedha.

Kulingana na hati ya mashtaka, washukiwa hao, pamoja na wengine ambao hawakuwa mbele ya mahakama, wanadaiwa kula njama kati ya Oktoba 2024 na Mei 2025 kuilaghai SHA shilingi milioni 17,591,473 kwa kuwasilisha madai ya kimatibabu yaliyoghushiwa chini ya Kliniki ya Kimatibabu ya Archprime huko Oyugis, Kaunti ya Homa Bay.