Licha ya baadhi ya wakulima wa kahawa katika Kaunti ya Bungoma kuendelea kuuzia mazao yao nchini Uganda wakidai kupata bei ya juu zaidi, baadhi ya vyama vya ushirika katika kaunti hiyo vinapanga kuanzisha miradi mipya ili kuongeza mapato yatakayowezesha malipo bora kwa mkulima.
Akihutubu kwenye mkutano mkuu wa mwaka (AGM) wakati wa kuwasilisha makadirio ya bajeti ya mwaka wa kifedha 2025/2026, Afisa Mkuu Mtendaji wa Chama cha Ushirika cha Kimama katika eneo bunge la Mlima Elgon, Ben Mulupi, amesema miradi kama vile ufugaji wa kuku na ng’ombe wa maziwa inaweza kusaidia chama kupata fedha zaidi zitakazowezesha wakulima kulipwa kwa viwango vinavyostahili.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa chama hicho, Benard Nyongesa, amesema kuwa licha ya changamoto ya biashara ya magendo ambayo kulingana naye inaendelea bila kudhibitiwa na vyombo vya usalama, wanalenga kuboresha kilimo cha kahawa kupitia mafunzo na uhamasishaji kwa wakulima.