Kenya imepokea shehena ya awali ya dozi 21,000 za mwanzo za Lenacapavir, dawa ya muda mrefu ya kujidunga VVU kabla ya kuambukizwa (PrEP), kuashiria hatua kubwa katika juhudi za taifa hili kukabiliana na maambukizi mapya ya virusi vya HIV.

Mkurugenzi Mkuu wa Afya Dkt Patrick Amoth alipokea shehena hiyo, akielezea kuchaguliwa kwa Kenya kati ya nchi za kwanza Afrika Mashariki kusambaza dawa hiyo kama uthibitisho wa utayari wa nchi kuchukua mikakati ya kibunifu ya kuzuia virusi vya ukimwi.

lenacapavir ni dawa ya muda mrefu ya kurefusha maisha iliyoundwa kwa watu wazima walio na ukimwi.
Maafisa wa afya walisisitiza kuwa si chanjo bali ni dawa ya kinga inayotolewa kila baada ya miezi sita au mara mbili kwa mwaka, na wagonjwa wataipata kwa Ksh.7,800 kwa mwaka.

Dawa hiyo iliidhinishwa na Utawala wa Chakula na Dawa wa Marekani mnamo Juni 2025 na baadaye kupitishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).

Mnamo Januari 2026, Bodi ya Dawa na Sumu ya Kenya (PPB) ilikamilisha ukaguzi wa kisayansi na kupendekeza usajili wake kwa matumizi ya kitaifa.

Shehena hiyo imewasilishwa kwa msaada kutoka Global Fund. Vipimo vingine 12,000 vya kuendelea vinatarajiwa kufikia Aprili, wakati Marekani imetoa dozi 25,000 za ziada ili kuimarisha utekelezaji wa mapema.