Seneta wa Trans Nzoia Allan Chesang ametupilia mbali kuhusishwa na kesi ya ulaghai iliyohusisha washukiwa saba waliokamatwa katika Harambee House.
Hii ni baada ya ripoti ya gazeti la humu nchini siku ya Ijumaa kudai kuwa washukiwa hao waliwahadaa raia wawili wa kigeni, Talal Yousef Yousef Zaitoun na kaka yake Hatem Youssef Yousef Zaitoun – wawakilishi wa kampuni ya Uswidi ya Jokara AB – katika mkataba wa uwongo wa zabuni uliohusisha usambazaji wa magari 500 ya Toyota Hiace High Roof.
Ripoti hiyo ilidai kuwa washukiwa wawili walikuwa wameajiriwa katika afisi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani Raymond Omollo, huku wengine wawili wakisemekana kuwa wasaidizi wa Seneta Chesang.
Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) hapo awali ilitupilia mbali madai kwamba maafisa wa serikali walihusika katika kesi ya ulaghai, ikizitaja ripoti hizo kuwa za kupotosha na za kushtua.
Seneta Chesang sasa pia amekanusha kuwa ana ujuzi wowote kuhusu, au kushirikiana na washukiwa hao wanaosemekana kuhusishwa na afisi yake.
Kupitia mawakili wake, kiongozi huyo alipinga kuhusika kwa afisi yake, akitaja madai hayo kuwa ni ya nia mbaya na ya kukashifu.
Idara hiyo iliongeza kuwa uchunguzi zaidi ulibaini kuwa walitumia Harambee House kulaghai wawekezaji wa kigeni baada ya kuingia kinyume cha sheria katika chumba cha mikutano cha ghorofa ya 12.
Watuhumiwa hao walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Milimani Machi 16, 2026, ambapo walikabiliwa na mashtaka mengi yakiwamo ya kula njama ya utapeli, kujipatia fedha kwa njia za uongo, kujipatia fedha za uhalifu na kughushi.
Walikana mashtaka na waliachiliwa kwa bondi ya Ksh.3 milioni kila mmoja au dhamana mbadala ya pesa taslimu Ksh.300,000, huku wadhamini wawili wakihitajika. Pasipoti zao zilikabidhiwa kortini.
Kesi hiyo imepangwa kutajwa Aprili 1, 2026.