Idara ya Upelelezi na uchuunguzi wa makosa ya Jinai (DCI) imeanzisha uchunguzi kuhusu kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Lugari Cyrus Jirongo, aliyefariki kufuatia ajali mbaya ya barabarani Jumamosi, Desemba 13, 2025.
Kulingana na DCI, ajali hiyo mbaya ilitokea katika eneo la Karai kando ya barabara kuu ya Nakuru-Naivasha, iliyohusisha gari la Jirongo na basi la huduma ya umma (PSV), linaloendeshwa na Kampuni ya Climax Limited.
Matokeo ya awali yanaonesha kuwa ajali hiyo ilihusisha mgongano wa ana kwa ana.
DCI inasema timu ya pamoja ya wapelelezi wa mauaji na wataalam wa mahakama kutoka Maabara ya Kitaifa ya Uchunguzi ilitumwa kwenye eneo la tukio, ambapo walifanya uchunguzi wa awali na kupata vielelezo muhimu.
Wakati huo uo walipata picha za CCTV kutoka Kituo cha Petroli cha Eagol, ambacho tangu wakati huo kimefanyiwa uchunguzi wa awali.
Polisi wanasema kuwa kanda hiyo inaonyesha Jirongo aliingia katika kituo cha mafuta saa 2:18:40 asubuhi kutoka upande wa Nairobi lakini hakutumia mafuta.
Saa 2:19:10 asubuhi, alisimama kwenye njia ya kutokea ya kituo kabla ya kugeuka kulia saa 2:19:19 asubuhi, akiendesha gari kurudi Nairobi. Muda mfupi baadaye, saa 2:19:25 asubuhi, CCTV ilinasa basi la PSV likigonga gari lake.

Maafisa wa upelelezi wamemhoji dereva wa PSV, Tyrus Kamau Githinji, ambaye awali alikuwa amerekodi taarifa katika kituo cha trafiki cha Naivasha na Aaiachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu akisubiri uchunguzi zaidi wa kosa la kusababisha kifo kwa kuendesha gari na anatakiwa kuripoti katika Kituo cha Trafiki cha Naivasha mnamo Desemba 22, 2025, kwa hatua zaidi.
Maafisa wa upelelezi pia wamerekodi taarifa kutoka kwa mlinzi wa usiku wa kituo cha mafuta na mhudumu wa mafuta, ambao wote walishuhudia matukio kabla ya ajali.
DCI ilisema kuwa uchunguzi unaendelea, huku timu ya uchunguzi ikitarajiwa kurejea eneo la tukio kwa uchunguzi zaidi

Maafisa wa upelelezi pia wanachunguza mienendo ya Jirongo kabla ya ajali, ikiwa ni pamoja na kurekodi taarifa za watu aliowasiliana nao usiku husika, hasa wale waliokuwepo wakati wa mkutano katika Baa na Mkahawa wa Karen Oasis, Nairobi.
Mbunge huyo wa zamani wa Lugari atazikwa nyumbani kwake Lumakanda Jumanne, Desemba 30.