Timu ya Faroe Islands iliiadhibu timu ya taifa ya Jamhuri ya Czech kwa ushindi wa magoli mawili kwa moja na kuzidisha matumaini yao ya kushiriki michuano ya kombe la dunia.
Faroe ambao wako katika nafasi ya 136 duniani kispoti, wako nafasi ya tatu wakiwa pointi moja nyuma ya Jamhuri ya Czech iliyo nafasi ya pili, huku mchezo mmoja pekee ukiwa umesalia katika kinyang’anyiro cha kufuzu hatua ya mchujo kwa fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazoandaliwa bara la Amerika Kaskazini.
Ushindi huo ulikuwa wa tatu mfululizo kwa Faroe, na hadi sasa hawajapoteza mchezo wowote kwa tofauti ya zaidi ya bao moja katika Kundi L.
Hata hivyo, bado wanahitaji ushindi mwezi ujao watakapokutana na vinara Croatia tarehe 14 Novemba, huku Jamhuri ya Czech wakimalizia kampeni yao kwa kumenyana na Gibraltar.
Iwapo watafuzu kushiriki kombe la dunia mwaka ujao,timu ya taifa ya Faroe itakuwa imevunja rekodi kwa kuwa timu ya kwanza kabisa kutoka taifa dogo zaidi kuwahi kufuzu Kombe la Dunia.
Picha/Hisani/Getty Images