Wakazi katika mtaa wa mabanda wa Cheposait viungani mwa mji wa Makutano kaunti ya Pokot magharibi, wanaitaka serikali ya kaunti kuelekeza mabomba ya maji kutoka uwanja wa michezo wa Makutano unaokarabatiwa katika sehemu zingine badala ya makaazi ya wananchi.

Wakizungumza na kituo hiki,wakazi hao wanadai kuwa,maji yamekuwa yakiingia katika majumba yao na hatua hazijachukuliwa kurekebisha hali hiyo.

Baadhi ya wakazi wa mtaa huo sasa wamelazimika kuondoka katika nyumba zao za kukodi na kutafuta hifadhi kwingine kutokana na wingi wa maji katika majumba yao.

Hofu ya wakazi hao ni mkurupuko wa ugonjwa wa kipindupindu ambao wanahofia inaweza kuzuka wakati wowote kutokana na mazingira duni ya mtaa huo wa mabanda.

Walioathirika zaidi ni watu wanaoishi na ulemavu.