Jumla ya watahiniwa 1,180 waliofanya mtihani wa KCSE 2025 hawatapokea matokeo yao baada ya Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) kuwafutilia mbali kwa kuhusika na makosa ya mtihani.
Akizungumza wakati wa kutolewa kwa matokeo ya KCSE ya mwaka wa 2025 katika Shule ya Upili ya AIC Chebisas mjini Eldoret, Waziri wa Elimu Migos Ogamba amebainisha kuwa hatua hiyo ilichukuliwa kufuatia kukamilika kwa uchunguzi ulioanza Novemba mwaka jana.
Alitetea uamuzi huo, akirejelea Kanuni za KNEC (Kushughulikia Makosa ya Mitihani) za 2015, Notisi ya Kisheria nambari 132 ya 2015, ambayo huipa Baraza mamlaka ya kisheria ya kusimamisha au kuzuia matokeo ya mtahiniwa kutokana na makosa ya mtihani.
Watahiniwa 840 walifutiliwa mbali matokeo ya mtihani wa KCSE wa 2024, huku matokeo 2,829 yakizuiliwa wakati huo.