Tume ya Maadili na Kupambana na ufisadi nchini(EACC) imemkamata na kumfikisha mahakamani mfanyakazi wa zamani wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), kwa madai ya kutumia cheti  kilichoghushiwa ili kupandishwa cheo.

Kulingana na tume hiyo, Lukaa Musamali Mukimi aliwasilisha cheti cha Shahada ya Sanaa katika Masomo ya Kijamii (Utawala wa Umma) cha kughushi, kinachodaiwa kutolewa na Chuo Kikuu cha Moi, ili kupata cheo katika IEBC.

Kufuatia uchunguzi uliofanywa na EACC, ilibainika kuwa hati hiyo ya kitaaluma ilikuwa ya kughushiwa na kwamba mshukiwa aliiwasilisha kimakusudi kama halisi.

Mukimi alikamatwa mnamo Novemba 19, 2025, na kufikishwa mahakamani siku moja baadaye kwa mashtaka ya kughushi kinyume na Kanuni ya Adhabu na Sheria ya Kupambana na Rushwa na Uhalifu wa Kiuchumi, Nambari 3 ya 2003.

Akifika mbele ya Mahakama ya Kupambana na ufisadi ya Milimani, Mukimi alikana mashtaka yote na akaachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu ya Ksh.200,000 au dhamana mbadala ya Ksh.500,000 akiwa na mdhamini mmoja wa kiasi kama hicho.