Mbunge wa Sigor Peter Lochakapong sasa anapendekeza kubuniwa kwa kamati za ardhi katika maeneo yaliyothibitishwa kuwa na madini katika kaunti ya Pokot Magharibi.

Akizungumza katika kijiji cha Tumeighyo ,wadi ya Masol,mbunge huyo amesema kupitia kamati hizo,shuguli za uchimbaji madini zitaendeshwa kwa utaratibu na kuzuia migogoro kwenye matimbo.

Aidha,amesema kwamba,shuguli hizo ni sharti zizingatie masuala ya mazingira ili kuzuia mmomonyoko wa udongo katika eneo hilo lililoripoti kuwepo kwa dhahabu.

Hayo yakijiri,mbunge wa Kapenguria Samuel Moroto amewataka wakazi wanaoishi karibu na maeneo yaliko madini kuzingatia usawa na kuishi kwa amani.

Moroto amesema,ni kupitia amani tu ambapo shuguli za uchimbaji wa dhahabu zitaendelea bila vikwazo na kuwatolea mwito raia kushirikiana na asasi za usalama katika eneo hilo.

Matamshi yake yanajiri siku chache tu baada ya watu wawili kuuawa katika mpaka wa kaunti za Pokot Magharibi na Turkana.

Kwingineko,seneta wa kaunti ya Turkana James Lomenen ameitaka serikali kuweka mipaka halisi baina ya kaunti Jirani ili kuzuia wakazi kuvuka upande wa pili bila uelewa na kuvua vurugu.

Aidha,amesema,wakati umewadia kwa serikali kuwahakikishia wakaazi wa maeneo ya mipaka usalama .