Rais William Ruto amemteua aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka ya kitaifa ya usalama barabarani NTSA Francis Meja kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma (PSC).
Uteuzi huo, uliotolewa kupitia Notisi ya Rais , umewasilishwa kwa Bunge ili kuzingatiwa na kuidhinishwa na Bunge.
Kwa sasa Meja anahudumu kama Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Umma, jukumu alilochukua Januari 2025.
Hapo awali alihudumu kama Mkurugenzi Mkuu mwanzilishi wa NTSA, ambapo aliongoza kuanzishwa kwa mamlaka hiyo na kutekelezwa kwa mageuzi ya usalama wa usafiri. Rekodi yake ya utumishi wa umma pia inajumuisha nafasi ya Msajili wa Magari katika Wizara ya Uchukuzi.

(Francis meja aliyeteuliwa kuhudumu kama mwenyekiti a tume ya utumishi wa umma)
Meja amewahi kuwa mjumbe wa baraza la Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Murang’a, akiongeza uzoefu wake katika uongozi wa taasisi na usimamizi wa sekta ya umma.
Bunge sasa litapeleka uteuzi wake kwa kamati husika ili kuhakikiwa kwa kuzingatia Katiba na Sheria ya Uteuzi wa Umma. Kamati itafanya kikao cha umma ili kutathmini sifa zake, uzoefu, uadilifu, na uwezo wake katika nafasi hiyo.
Kisha kamati itawasilisha ripoti mbele ya Bunge ikipendekeza kuidhinishwa au kukataliwa kwa uteuzi huo. Wabunge watajadili na kuipigia kura ripoti hiyo, na baada ya hapo matokeo yatawasilishwa kwa Rais kwa uteuzi rasmi au hatua zaidi.