Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja, ameahidi kuwa serikali itaendelea kuunga mkono familia za maafisa walioaga wakiwa kazini , alitoa hakikisho hilo Alhamisi, Desemba 4, 2025, alipokuwa akiongoza ibada ya 7 ya kila mwaka ya ukumbusho wa mashujaa waliokufa wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) na Huduma ya Magereza ya Kenya.
Katika hotuba yake kwa maafisa waliopoteza maisha wakiwa mstari wa mbele, Kanja amesisitiza umuhimu wa kuwakumbuka na kuwaenzi wale “ambao ushujaa wao ulilinda amani na utulivu wa Kenya”.
Kadhalika Kanja amesisitiza dhamira ya serikali ya kuendeleza Muswada wa Mashujaa wa Jeshi la Polisi na Mashujaa Walioaga, unaolenga kuwatambua rasmi maafisa waliostaafu na kushughulikia mahitaji ya ustawi wa familia za maafisa waliofariki wakiwa kazini.
Hafla hiyo iliyofanyika katika Chuo cha Taifa cha Polisi Kampasi ya Embakasi ‘A’, imewakutanisha viongozi wakuu, maaqfisa, washirika na familia katika mkusanyiko adhimu wa kuwaenzi wanausalama waliopoteza maisha wakati wakitumikia taifa.