Wizara ya Jinsia, Utamaduni na Huduma za Watoto imetoa Ksh.877,608,000 kusaidia familia zisizojiweza kote nchini chini ya mpango wa Fedha kwa Mayatima na Watoto Wanaoishi Katika Mazingira Hatarishi (CT-OVC).
Malipo hayo, yatafaidi boma 438,804 zilizosajiliwa chini ya mpango wa Inua Jamii, huku kila boma inayofaidika ikipokea Ksh.2,000 kwa kipindi cha malipo cha Novemba 2025. Kulingana na Idara ya Huduma za Watoto, malipo yataanza Ijumaa, Januari 9, 2026 kupitia Mtoa Huduma ya Malipo aliye na kandarasi.
Mpango wa CT-OVC unawakilisha juhudi kubwa za serikali za kuimarisha huduma za kijamii kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu. Mpango huo unalenga kuhimiza familia na jamii kuwalea na kuwahifadhi watoto yatima na walio katika mazingira magumu huku wakati huo huo wakikuza maendeleo yao kwa ujumla.