Vyombo vya usalama katika Kaunti ya Uasin Gishu vimewakamata washukiwa watatu na kurejesha bunduki aina ya AK-47, wiki moja baada ya tukio la uhalifu lililosababisha kifo cha mfanyakazi wa kaunti.
Kamishna wa Kaunti hiyo Benjamin Mwanthi amesema operesheni hiyo ilifanikiwa kupitia ushirikiano wa Polisi wa Taifa, DCI na waendesha boda boda.
Polisi wanasema washukiwa hao wanahusishwa na visa vya uporaji katika maeneo ya Moiben, Kapseret, Ainabkoi, Kesses na Turbo, wakitumia pikipiki kufanya uhalifu huo, Bunduki hiyo yenye risasi kumi imepelekwa kufanyiwa uchunguzi .
Wakati huo huo, operesheni dhidi ya pombe haramu na dawa za kulevya zimeimarishwa, washukiwa 96 wakikamatwa. Serikali imewahakikishia wananchi usalama huku ikiwataka waliodhulumiwa kujitokeza kutoa taarifa.