Watu watatu wakiwemo watoto wawili waliteketea hadi kufa katika kijiji cha Bulagu huko Budalang’i kaunti ya Busia baada ya nyumba waliyokuwa wamelala kushika moto usiku wa kuamkia Jumamosi.
Kulingana na jirani wa marehemu, alisikia vilio vya kuomba msaada mwendo wa saa moja asubuhi. Alipokimbilia nyumbani kwa Patrick Bahati, alikuta tayari moto umeenea sana.
Juhudi za kuwaokoa Bahati na watoto wake wawili waliokuwa darasa la saba na darasa la pili mtawalia hazikufua dafu kutokana na kukithiri kwa moto huo.
OCPD wa Kaunti Ndogo ya Bunyala Lawrenias Odinga alithibitisha kisa hicho, akisema uchunguzi kuhusu chanzo cha moto huo, ambao bado haujajulikana, tangu sasa umeanzishwa.
Miili ya marehemu ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Port Victoria.