Waziri wa Uchukuzi David Chirchir ametoa wito kwa madereva, wazazi na walezi kutanguliza usalama wa watoto barabarani shule zitakapofunguliwa kwa muhula wa kwanza.

Chirchir ameonya kuwa kurejea kwa wanafunzi shuleni kutaongeza idadi ya trafiki kote nchini, na hivyo kuongeza hatari ya ajali za barabarani ikiwa tahadhari haitazingatiwa.

Katika ujumbe wake, waziri huyo amesisitiza kwamba kufunguliwa kwa shule kunakuja na uwajibikaji wa pamoja.

Amebainisha kuwa maelfu ya wanafunzi watakuwa wakisafiri kila siku, iwe kwa miguu au kwa gari, na kutoa wito kwa watumiaji wote wa barabara kuwajibika ili kuzuia majanga yanayoweza kuepukika.