Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo imetoa ruzuku kwa bei ya mbegu za mahindi kwa msimu ujao wa upanzi, kama sehemu ya juhudi za serikali za kuimarisha usalama wa chakula nchini kote.
Katika taarifa Katibu Mkuu Dkt Kipronoh Ronoh alifichua kuwa serikali imetenga Ksh.2 bilioni kutoa ruzuku kwa mbegu za mahindi kwa mwaka wa kifedha wa 2025/2026.
Mpango huo unalenga kufanya mbegu bora za mahindi kuwa nafuu zaidi kwa wakulima kote nchini, kuhakikisha ongezeko la uzalishaji na upatikanaji wa chakula dhabiti.
Kulingana na miongozo mipya, bei za ruzuku zimewekwa kwa Ksh.250 kwa Kilo 1, Ksh. 500 kwa Kilo 2, Ksh.2,500 kwa kilo 10, na Ksh.6,000 kwa mfuko wa kilo 25.

Marekebisho haya, Wizara ilisema, yanaanza kutumika mara moja na yanatarajiwa kuwapunguzia wakulima mzigo wa kifedha katika msimu wa kupanda.
Dk Ronoh alisisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kuwawezesha wakulima wadogo na kuongeza uzalishaji wa kilimo.