HARAKATI ZA UCHIMBAJI DHAHABU KAPUNIA ZAWACHA MASHIMO HATARI NA YASIYOTUMIKA MASOL KATIKA KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI.

Kijiji cha Kapunia huko Masol, Kaunti ya Pokot Magharibi, ambacho hapo awali kilikuwa na shughuli nyingi za uchimbaji madini, sasa kimebaki kama kijiji kisicho na watu baada ya kuporomoka kwa shughuli za uchimbaji dhahabu zilizovutia maelfu ya familia za wafugaji eneo hilo.

Ugunduzi wa dhahabu miaka kadhaa iliyopita ulisababisha wimbi kubwa la watu kuhamia Kapunia, huku familia za wafugaji zikihama na mifugo yao kutafuta madini hayo ya thamani. Kwa miaka mingi, wachimbaji walimiminika eneo hilo wakitarajia kutajirika kutokana na akiba ya dhahabu iliyokuwepo.

Hata hivyo, akiba ya dhahabu ilipungua taratibu, jambo lililowalazimu wakazi wengi kuondoka kijijini hapo na kurejea makwao ya asili. Wengine walihamia maeneo kama Romos, Kambi Karaya na Katikomor, ambako wanaendelea kutafuta dhahabu.

Leo hii, hali ya Kapunia ni tofauti kabisa. Kijiji hicho kimebaki karibu tupu, kikiwa na mazingira makavu na tasa, pamoja na maeneo mengi ya uchimbaji yaliyoachwa wazi na kutotumiwa tena. Mashimo marefu yaliyoachwa wazi na wachimbaji yamekuwa tishio kubwa kwa jamii ya eneo hilo.

Mashimo hayo yaliyoachwa wazi hayachangii tu uharibifu wa mazingira bali pia yanahatarisha sana maisha ya mifugo. Wiki iliyopita, ngamia mmoja anaripotiwa kutumbukia kwenye mojawapo ya mashimo hayo marefu wakati akichunga, jambo lililozua hofu mpya miongoni mwa wakazi kuhusu hatari zinazosababishwa na maeneo hayo ya uchimbaji yaliyoachwa.

Sasa wakaazi wakiongozwa na Richard cherelmot, wanaiomba serikali kuchukua hatua za haraka kuhakikisha kuwa mashimo hayo yaliyoachwa wazi yanazibwa au kulindwa ipasavyo ili kuzuia ajali zaidi. Wana hofu kuwa bila hatua za haraka, mifugo zaidi inaweza kutumbukia kwenye mashimo hayo, jambo litakalo-athiri maisha na kipato cha familia za wafugaji.

Jamii pia chini Samuel Nakori, naibu Chifu Lokesheni ya Masol inaelezea wasiwasi wake kuhusu mvua zinazotarajiwa za el niño, ikionya kuwa mvua kubwa inaweza kuzidisha hali hiyo. Wanasema maji yanaweza kujaza mashimo hayo marefu, na kuyafanya kuwa vigumu kuonekana, hali inayoongeza hatari kwa mifugo na binadamu.

Wakati kapunia ikiendelea kukabiliana na matokeo ya kipindi hicho cha uchimbaji dhahabu, wakazi wanataka serikali na mamlaka husika kutathmini maeneo hayo ya uchimbaji yaliyoachwa, kurejesha hali ya mazingira yaliyoharibiwa, na kuchukua hatua za haraka kulinda jamii na mifugo yake dhidi ya hatari zaidi.

APERIT FM, HII NI YETU