Huduma za afya nchini zinatarajiwa kutatizika baada ya Muungano wa Vyama Vya Wafanyikazi wa Sekta ya afya kutangaza mgomo wa Kitaifa kuanzia Julai 20 mwaka huu.
Katika taarifa yao muungano huo umesema serikali imeshindwa kushughulikia malalamishi ya muda mrefu ya wahudumu wa afya.
Vyama hivyo pia vimeishtumu baraza la magavana COG, kwa madai ya kutotekeleza madai yaliyowasilishwa Juni 15, yakiwamo kuboresha masilahi ya wafanyikazi, kuwaajiri kwa masharti ya kudumu wahudumu wa afya kwa wote UHC, pamoja na Global Fund, pamoja na kuwapa barua za ajira.
Vilevile vyama hivyo vinataka Kaunti zote kutia saini na kutekeleza mkataba wa pamoja wa masharti ya ajira CBA, Kutekeleza makubaliano ya kurejea kazini, yaliyotiwa saini Januari 28, na kutia saini mikataba ya utambuzi wa vyama vya wafanyikazi.
Hata hivyo viongozi wa vyama hivyo wamesema wako tayari kwa mazungumzo wakiitaka serikali ya kitaifa na zile za kaunti kuharakisha majadiliano ili kupata suluhu kabla ya mgomo huo kuanza.

