Rais William Ruto ametangaza kuwa wanafunzi wote watakao faulu katika mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne KCSE, nakupata nafasi katika vyuo vikuu na vyuo vya kati sasa watapata ufadhili kamili wa serikali katika kufadhili masomo yao.
Akizungumza katika Ikulu ya Nairobi, rais Ruto amesema sera hiyo mpya itaanza kutekelezwa Septemba mwaka huu, baada ya bunge kupitisha mswada mpya wa mfumo mpya wa ufadhili wa elimu ya juu.
Rais amesema ufadhili huo utatolewa kwa wanafunzi wote wanao kidhi vigezo vya kujiunga na vyuo vikuu na vya kati, bila kujali hali yao ya kifedha, akishikilia kuwa wazazi na walezi, watakao amua kugharamia masomo ya wanao watafanya hivyo kwa hiari.
Hatua hiyo inatarajiwa kuchukua nafasi ya mfumo wa sasa wa ufadhili unaotoa ufadhili wa mikopo kulingana na kiwango cha mahitaji ya kifedha ya kila mwanafunzi.

