Waziri wa elimu Julias Migos Ogamba, amesema kucheleweshwa kwa fedha za ufadhili wa serikali kwa Dhule, Vyuo vya kiufundi, TVET pamoja na Vyuo Vikuu vya umma, kunatokana na upungufu wa fedha katika bajeti na kucheleweshwa kwa utoaji wa fedha kutoka wizara ya fedha.
Akizungumza mbele ya kamati ya Bunge la kitaifa ya uwekezaji wa umma, kuhusu utawala na elimu, waziri Ogamba amesema wizara ya elimu haijazuia fedha hizo kimaksudi bali inakabiliwa na pigo kubwa la ufadhili kutokana na mgao wa bajeti finyu anayosema ni chini ya mahitaji halisi ya sekta ya elimu.
Ogamba amesema kwa sasa sekta ya vyuo vikuu vya umma inakabiliwa na kesi ya shilingi bilioni 29, hali inayotatiza utoaji wa ufadhili kwa wanafunzi na waendeshaji wa taasisi hizo.
Kwa mujibu wa Ogamba, serikali iliitaji zaidi ya shilingi bilioni 70, kufadhili masomo na kutoa ruzuku kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, lakini ilipokea takribani shilingi bilioni 41 pekee, hivyo kusababisha pengo kubwa la fedha.
Kamati hiyo ya Bunge la kitaifa ya uwekezaji wa umma, pia imeitaka wizara ya elimu, kuchukua hatua dhidi ya wakuu wa baadhi ya taasisi za elimu wanao daiwa kutumia vibaya fedha za umma na kuwatoza wazazi ada kinyume na miongozo ya wizara hiyo ya elimu nchini.

