Inasubiriwa kuona iwapo Gavana wa Kajiado, Joseph Ole Lenku na Mbunge Maalum, Joseph Wainaina watafika mbele ya Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano, NCIC Septemba 17 kuhojiwa kuhusiana na kauli zenye utata wanazodaiwa kutoa huku tume hiyo ikiendelea kunoa makali yake dhidi ya viongozi wanaodaiwa kutoa matamshi ya uchochezi na ukabila.
NCIC imemwagiza Gavana Lenku kufika mbele yake kutokana na matamshi yake ya kushinikiza watu wa jamii moja kuvitwaa viti vya kisiasa kwenye kaunti za Kajiado na Narok wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka ujao. Katika taarifa, NCIC imeonya kwamba kwamba kutotiii maagizo hayo kunaweza kusababisha kutolewa kwa agizo la kukamatwa kwa gavana huyo wa Kajiado.
Lenku ametakiwa kufika mbele ya NCIC Septemba 17 mwaka huu ili kusaidia katika uchunguzi unaoendelea kuhusu matamshi aliyodaiwa kutoa huko Ewuaso Oonkidong’a kwenye eneo la Kajiado Magharibi mnamo Agosti 22.
Aidha Mbunge Maalum, Joseph Wainaina ametakiwa kufika mbele ya NCIC kuhojiwa kutokana na matamshi anayodaiwa kuyatoa wakati wa mkutano wa umma kwenye eneo la Ngeria huko Uasin Gishu mnamo Agosti 29.
Matamshi hayo yanadaiwa kuashiria kwamba watu wa jamii moja ambao hawaungi mkono kuchaguliwa tena kwa Rais Ruto wanapaswa kuondoka katika Kaunti ya Uasin Gishu.
NCIC imesema inachunguza matamshi hayo chini ya vifungu vya Sheria ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa vinayohusiana na matamshi ya chuki, ukabila na mwenendo unaoweza kudhoofisha utangamano miongoni mwa jamii.
Tume imemwonya kwamba kutoheshimu wito wa viongozi hao kufika mbele yake kunaweza kusababisha kutolewa kwa agizo la kukamatwa kwao na kufunguliwa mashtaka.
Siku ya Jumanne, Waziri wa Huduma za Umma, Geoffrey Ruku pia alifika mbele ya NCIC kuhojiwa kuhusu madai ya kutoa matamshi ya chuki.
Naibu Mwenyekiti wa NCIC,Irene Chepoisho amesema kwamba wiki ijayo tume hiyo itatoa ripoti kuhusu uchunguzi iliyofanya.
Viongozi wengine ambao awali wamewekwa kwenye rada ya NCIC ni Mbunge wa Mukurweini John Kagucia, Gavana wa Busia Paul Otuoma, Mbunge wa Homabay Mjini, Peter Kaluma vilevile Kiongozi wa Chama cha DCP, Rigathi Gachagua huku wananchi na viongozi mbalimbali wa kijamii wakiendelea kushinikiza kudumishwa kwa amani kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
APERIT FM, HII NI YETU

