Waziri wa usalama Onesimus Kipchumba Murkomen, amezindua rasmi mfumo wa kisasa wa utambuzi wa alama za kibayometriki unaolenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kuharakisha mchakato wa kupata cheti cha kutokuwa na rekodi ya uhalifu, maarufu kama good conduct.
Kupitia teknolojia hiyo, muda wa kusubiri cheti hicho umepunguzwa kutoka siku 14 zilizokuwa zikitumika awali, hadi saa 24 pekee.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri Murkomen amesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali za kuimarisha utoaji wa huduma kwa kutumia teknolojia ya kisasa, kuongeza ufanisi katika shughuli za usalama na kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa haraka na kwa urahisi zaidi.
Mfumo wa MBIS unatarajiwa pia kuboresha usahihi wa utambuzi wa taarifa za watu, kuimarisha uchunguzi wa makosa ya jinai na kusaidia taasisi za usalama kutoa huduma zinazokidhi viwango vya kimataifa.

