You are currently viewing JUBILEE YAMJIBU VIKALI RAIS WILLIAM RUTO KUFUATIA KAULI ZAKE KWA UHURU KENYATTA

JUBILEE YAMJIBU VIKALI RAIS WILLIAM RUTO KUFUATIA KAULI ZAKE KWA UHURU KENYATTA

Chama cha Jubilee kimemjibu vikali rais William Ruto kufuatia kauli zake za kumkosoa aliyekuwa rais Uhuru Kenyatta, na kumhusisha na ufadhili wa shughuli za upinzani.

Katibu mkuu wa chama cha Jubilee Moitalel Ole Kenta, amesema serikali ambayo imekuwa madarakani kwa miaka minne, haiwezi kuendelea kumlenga mtu aliyeondoka ikulu mwaka 2022.

Ole Kenta amemtaka rais Ruto kuwacha kumfanya Uhuru Kenyatta kuwa kiini cha mashambulizi yake ya kisiasa, na badala yake awajibike kuhusu rekodi ya serikali yake katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Jubilee imesema Uhuru ambaye alistaafu kutoka uwongozi wa urais mwaka wa 2022, ana haki kama mkenya kutoa maoni yake na kushiriki katika maswala ya kisiaasa.

Chama hicho pia kimeikosoa serikali ya rais Ruto kwa kuendelea kumhusisha Uhuru na maswala ya sasa, badala ya kujikita katika changamoto zinazowakabili wakenya, zikiwemo gharama ya maisha, kodi na ukosefu wa ajira.

Jubilee kinasema mjadala wa kisiasa unapaswa kulenga utendaji na mipango ya viongozi walio madarakani na wale wanatafuta kuunda mstakabali wa Kenya, badala ya kuendelea kumweka mbele rais mustaafu Uhuru Kenyatta.

Mvutano huo unajiri wakati shughuli za kisiasa zikizidi kupamba moto kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027, uku viongozi wa Kenya Kwanza wakizidi kumhusisha Uhuru na vuguvugu la Linda Mwananchi na shughuli za upinzani.

Matamshi ya Jubilee yanafuata hatua ya rais William Ruto kumshambulia vikali Uhuru Kenyatta akimtuhumu kufadhili shughuli za upinzani katika juhudi za kuhujumu utawala wake.

Akizungumza na wakaazi wa Eldoret katika kaunti ya Uasin Gishu, rais Ruto, alidai kuwa Uhuru alishindwa kutekeleza kikamilifu baadhi ya ahadi wakati wa utawala wake zikiwemo mpango wa nyumba za bei nafuu na huduma ya afya kwa wote.

Rais alisema serikali yake inapaswa kuhukumiwa kutokana na rekodi yake ya kazi, akitaja miradi ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu, masoko na miundo msingi, kuwa baadhi ya miradi inayotoa ajira kwa vijana.

Ruto pia aliwahimiza vijana wanaofanya kazi katika miradi hiyo kujiandaa kwa fursa zaidi, akisema angependa miradi ya ujenzi kuendelea kwa miaka mingi iwapo atachaguliwa tena.

Madai ya Ruto si ya kwanza kwa wakenya kuanza kumtuhumu rais huyo mstaafu, kufadhili shughuli za vuguvugu la Linda Mwananchi linalo husishwa na seneta wa kaunti ya Nairobi Edwin Sifuna.

Sifuna hata hivyo wakati wote, amekuwa mwepesi wa kufutilia mbali tuhuma hizo, akikariri kuwa shughuli za vuguvuvu hilo zinafadhiliwa na wananchi wanaotaka magezi ya kisiasa nchini.

                                                                                                                                APERIT FM, HII NI YETU