Serikali ya kaunti ya Baringo imeyapandisha hadhi rasmi maeneo ya Marigat, Mogotio na Eldama-Ravin kuwa manisipaa, hatua inayo dhihirisha maafanikio makubwa ya maendeleo ya miji kwenye kaunti hiyo.
Akizungumza wakati wa kutoa rasmi maamlaka hayo, Gavana wa kaunti hiyo ya Baringo Benjamin Cheboi, ameeleza kuwa kupandishwa hadhi kwa miji hiyo mitatu, kutavutia ufadhili wa maendeleo, kutoka kwa benki ya maendeleo ya afrika, ili kuendeleza uboreshaji wa miundo mbinu.
Amebainisha kuwa barabara zilizoboreshwa, mifereji ya maji, taa za barabarani na maendeleo mengine, yatasaidia manispaa hizo kuwavutia zaidi wawekezaji na kubuni fursa za ajira kwa wakaazi wa eneo hilo.
Ni kauli ambayo imeungwa mkono na mbunge wa Baringo Kusini Charles Kamuren, ambaye amesema kupandishwa hadhi kwa miji hiyo, kunadhihirisha lengo la kaunti hiyo ya baringo la kuimarika kimaendeleo.
Amewahimiza wakaazi wa eneo hilo kushirikiana na serikali ya kaunti na ya kitaifa, ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inafanikishwa.

