Raia wa kigeni wanaoendesha biashara nchini Kenya wamepewa muda wa siku 90 kuhalalisha hali yao ya uhamiaji na shughuli zao za kibiashara.
Serikali inasema hatua hiyo inalenga kulinda fursa kwa wafanyabiashara wa Kenya huku ikihakikisha kuwa raia wa kigeni wanaofanya kazi kisheria wanalindwa.
Tangazo hilo lilitolewa Jumanne, Septemba 8, 2026, na Msemaji wa Ikulu, Hussein Mohamed.
Hatua hiyo inafuatia malalamiko yaliyotolewa na wafanyabiashara wa Kenya kuhusu kuongezeka kwa ushiriki wa raia wa kigeni katika biashara ndogondogo na biashara zisizo rasmi.
“Kenya inaendelea kukaribisha uwekezaji, shughuli za biashara na ajira halali kutoka nje ya nchi,” inasema taarifa iliyotiwa saini na Hussein Mohamed.
Serikali ilisema kuwa hatua hizo mpya zitatekelezwa kwa kuzingatia Katiba, sheria za Kenya na wajibu wa kimataifa wa nchi hiyo.
Rais William Ruto ameagiza kuwa Mswada wa Maudhui ya Ndani wa mwaka 2025 (Local Content Bill, 2025) uboreshwe ili kuweka kanuni zilizo wazi zaidi kuhusu ushiriki wa wageni katika biashara ndogondogo.
Mfumo huo unaopendekezwa utabainisha biashara na shughuli za kiuchumi ambazo zinaweza kutengwa mahususi kwa ajili ya raia wa Kenya.
Wakati huo huo, serikali inasema kuwa raia wa kigeni wenye haki halali ya kufanya kazi, kuwekeza au kuendesha biashara nchini Kenya wataendelea kulindwa.

