Serikali imepiga marufuku kampuni zote za kusaga miwa nchini kuagiza sukari kutoka nje ya nchi, ikisema hatua hiyo inalenga kuimarisha uzalishaji wa ndani na kuwalinda wakulima wa miwa.
Katibu wa Wizara ya Kilimo, Dkt. Kipronoh Ronoh, amesema Kenya kwa sasa ina uwezo wa kuzalisha sukari ya kutosha kukidhi mahitaji ya soko la ndani, hivyo hakuna ulazima wa kuendelea kuagiza bidhaa hiyo kutoka mataifa ya nje.
Kwa mujibu wa Dkt. Ronoh, marufuku hiyo itasaidia kuimarisha sekta ya sukari, kuongeza mapato ya wakulima wa miwa na kupunguza utegemezi wa sukari ya kutoka nje.
Alisisitiza kuwa serikali imejizatiti kuhakikisha wakulima wanapata faida kutokana na jasho lao na kwamba miwa inayozalishwa nchini inapewa kipaumbele kabla ya kufikiria uagizaji wa sukari.
Dkt. Ronoh alitoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa kampasi ya kumi ya Shule ya Kilimo nchini iliyofanyika katika eneo bunge la Seme, kaunti ya Kisumu.

