You are currently viewing SERIKALI YATANGAZA EBOLA KUWA UGONJWA HATARI WA MLIPUKO KENYA

SERIKALI YATANGAZA EBOLA KUWA UGONJWA HATARI WA MLIPUKO KENYA

Serikali imetangaza rasmi Ebola kuwa ugonjwa hatari wa mlipuko chini ya Sheria ya Afya ya Umma, ikianzisha kanuni mpya zinazosimamia ufuatiliaji wa magonjwa, uchunguzi, karantini na usimamizi wa maambukizi yanayoshukiwa. Tamko hilo hata hivyo halimaanishi kwamba Kenya imetangaza mlipuko wa ebola humu nchini lakini linatoa mfumo wa kisheria wa kutekeleza hatua za kuzuia na kudhibiti magonjwa.


Katika notisi maalum kupitia Gazeti Rasmi la Serikali, Waziri wa Afya Aden Duale ametangaza ugonjwa wa ebola unaosababishwa na virusi vya Bundibugyo kuwa ugonjwa hatari wa mlipuko chini ya Kifungu cha 35 cha Sheria ya Afya ya Umma.

Chapisho hilo limewekwa katika Notisi ya Kisheria Nambari 203.


Katika notisi tofauti, Notisi ya Kisheria Nambari 204, serikali ilichapisha Sheria za Afya ya Umma kuhusiana na ugonjwa wa ebola zinazoelezea hatua za kuzuia na kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.


Kanuni hizo zinaelezea kuhusu huduma za uchunguzi wa afya ya umma katika sehemu za kuingilia, tathmini ya kimatibabu ya visa vinavyoshukiwa, kutengwa na rufaa ya wagonjwa, pamoja na ufuatiliaji na karantini ya watu ambao huenda wameathiriwa na virusi hivyo.

Pia zinaeleza majukumu ya waendeshaji wa huduma za usafiri, ikiwa ni pamoja na vifungu vinavyohusiana na ukaguzi na usafi wa mazingira.


Chini ya mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa, kanuni hizo zinashughulikia mahitaji ya arifa kwa vituo vya afya, wataalamu wa matibabu na maabara, pamoja na uchunguzi na ufuatiliaji wa watu waliogusana na wagonjwa.


Sheria hizo pia zinatoa huduma za uteuzi wa vituo vya afya vinavyohusika katika kusimamia visa vya ebola na kuanzisha taratibu za kukagua na kusafisha majengo ambapo maambukizi yanaweza kutokea.

Kanuni hizo pia zinaangazia utunzaji wa mili ya watu wanaofariki dunia kutokana na ebola, ikiwa ni pamoja na mazishi kwa njia salama na ya heshima.


Vifungu vingine vinashughulikia mawasiliano ya umma na kampeni za uhamasishaji kupitia vyombo vya habari.
Aidha kulingana na kanuni zilizotangazwa, itakuwa ni kosa kupuuza maagizo halali ya karantini, kutoa taarifa za uongo au kumsaidia mtu kuepuka kutengwa.


Kanuni hizo pia zinahitaji visa vinavyoshukiwa kuripotiwa mara moja, kuwapa maafisa wa afya mamlaka ya kufuatilia watu waliogusana na kuzuia watu kutembea, na kuweka wazi jinsi watu wanaofariki dunia kutokana na ugonjwa huo wanavyopaswa kushughulikiwa na kuzikwa.


Kanuni hizi za kukabili ebola zinajiri huku kukiwa na ufuatiliaji mkubwa wa ugonjwa humu nchini kufuatia kifo cha mtu aliyeingia humu nchini kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huku masuali mengi yakiibuka kuhusu ni vipi alifaulu kuingia nchini licha ya kwamba ni wazi alikuwa kwenye hali mbaya ya kiafya.


Ebola ni ugonjwa wa virusi ambao unaweza kusababisha homa, udhaifu, kutapika, kuendesha na katika baadhi ya matukio kutokwa na damu ndani na nje ya mwili.


Virusi vya ugonjwa huo huenea kupitia kugusana moja kwa moja na damu au majimaji mengine ya mwili ya watu walioambukizwa.

APERIT FM, HII NI YETU