Katibu wa Idara ya Serikali ya Kazi za Umma na Maendeleo, Joel Arumonyang, amesema serikali imetenga rasilimali za kutosha kufanikisha ujenzi wa maabara katika shule 59 katika Kaunti ya Pokot Magharibi, katika mwaka huu wa kifedha.
Kulingana na Arumonyang, uwekezaji huo unalenga kuhakikisha kuwa, sawa na maeneo mengine nchini, wanafunzi wa Pokot Magharibi wanapata fursa ya kuimarisha ujuzi wao kupitia mafunzo ya vitendo.
Amesema Kenya inaendelea kuweka mikakati ya kufikia malengo ya kuwa taifa lenye hadhi ya juu kimaendeleo ifikapo mwaka 2060, akisisitiza kuwa uwekezaji katika elimu ni miongoni mwa hatua muhimu za kufanikisha azma hiyo.
Aidha, Arumonyang amewataka wakazi wa Kaunti ya Pokot Magharibi kutumia vyema mvua za El Niño zilizotabiriwa pamoja na ruzuku ya mbolea ili kuongeza uzalishaji wa chakula, hasa baada ya kipindi kirefu cha kiangazi.
Amesema serikali pia inaweka mikakati ya kuhakikisha wananchi wanapata msaada wa chakula iwapo kutatokea upungufu wa chakula kutokana na athari za ukame na mabadiliko ya hali ya hewa.
APERIT FM,HII NI YETU

