Siku chache baada ya maandamano ya wafanyabiashara wadogo wadogo jijini Nairobi, Rais William Ruto ameratibiwa kukutana nao leo katika Ikulu ya Nairobi baada ya kurejea kutoka Zambia ambako alihudhuria hafla ya kuapishwa kwa Rais Hakainde Hichelema kwa muhula wa pili jana.
Mkutano huo umetajwa kuwa wa kusikiliza malalamiko ya wafanyabiashara hao na namna ambavyo serikali inaweza kuingilia kati.
Wanapinga ongezeko la kiwango cha chini cha thamani kinachotumiwa na Mamlaka ya Ukusanyaji kodi nchini KRA, katika kukadiria ushuru kwenye mizigo ambayo wanaagiza kutoka nje ya nchi.
Kiwango cha chini cha thamani ya kontena la futi 40 kimepandishwa kutoka shilingi milioni mbili nukta tano hadi shilingi milioni tatu nukta mbili hali ambayo wanasema itaongeza gharama za uagizaji wa bidhaa na kuwapunguzia zaidi faida zao.
Hata hivyo utafiti umebaini kuwa baadhi ya wafanyabiashara wamekataa mwaaliko huo wakimtuhumu mwenyekiti wao Benson Mutahi kwa kutowajali.
Wanalalamika kuwa hakuonekana kwenye maandamano yao Ijumaa ilhali ni yeye amepanga mkutano wa Ikulu, wakidai amepanga mkutano baada ya kukutana na Mbunge mmoja mwenye ushawishi serikalini katika Kaunti ya Kiambu.
Wale ambao wamekataa mwaliko huo wanadai Mutahi hana nia ya kutatua changamoto za wafanyabiashara bali analenga tu kujinufaisha kupitia mkutano huo wa Ikulu.
Hata hivyo mwenyekiti huyo amekuwa akisajili majina ya wale ambao wako tayari kuenda Ikulu leo.
Rais anarejelea mikutano yake ya Ikulu baada ya mapumziko ya wiki kadhaa, mwezi jana alikutana na walinzi wa kibinafsi, wazee wa mitaa, maimamu miongoni mwa makundi mengine.
APERIT FM, HII NI YETU

