You are currently viewing UFARANSA YAITUPA NJE MOROCCO KWENYE KOMBE LA DUNIA

UFARANSA YAITUPA NJE MOROCCO KWENYE KOMBE LA DUNIA

Ufaransa imefuzu kucheza nusu fainali za Kombe la Dunia baada ya kuitupa nje Morocco kwa kuicharaza 2-0 kwenye robo fainali licha ya Kylian Mbappe kukosa mkwaju wa penati baada ya kuchezewa “rafu” na Noussair Mazraoui.

Hata hivyo Mbappe, nyota wa Real Madrid aliwanyanyua mashabiki wa Paris mnamo dakika ya 60 baada ya kuziona nyavu za Morocco kufuatia pasi ya Désiré Doué na kuipatia Ufaransa bao la kwanza.

Ousmane Dembele aliipatia Ufaransa goli la pili dakika sita baadae, kufuatia shuti kali lililomzidi nguvu mlinda lango wa Morocco Yassine Bounou.

Ufaransa kucheza nusu fainali na Uhispania ama Ubelgiji

Ufaransa sasa inajiandaa kukutana na ama Uhispania au Ubelgiji katika hatua ya nusu fainali, hii ikiwa ni mara ya tatu mfululizo kwa timu hiyo kwenye Kombe la Dunia na ambayo inawania kushinda taji lao la tatu. Ikumbukwe Les Bleus pia waliifungashia virago Ubelgiji katika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia la 2018.

Kocha wa Ufaransa Didier Deschamps alisema baada ya mechi hiyo kwamba sasa wamefika mahali walipotamani kufika na sasa wanapumzika wakisubiri kujua nani atakuwa mpinzani wao kwenye mchezo unaofuata.

Kocha huyo aidha amemmwagia sifa Mbappe ambaye tayari amefunga goli la nane kwenye michuano hii. Amesema hakuna tatizo anapokuwepo Kylian. Hajitilii shaka, ingawa alikuwa na nafasi nyingine kabla ya kufunga goli la kwanza, aliongeza wakati alipozungumza na kituo cha utangazaji cha M6.

Morocco yasifu uwezo wa Ufaransa, yaahidi kujiimarisha

Morocco, ambayo imeondolewa kwenye michuano hiyo wamesema imewalazimu kukubali matokeo hayo dhidi ya timu bora kabisa, ingawa walikuwa na matumaini makubwa ya kusonga mbele. Kocha wa Morocco Mohamed Ouahbi licha ya kukiri kushindwa lakini amesema kikosi chake kimeacha taswira nzuri kutokana na mchezo waliounyesha.

Hata hivyo amesema bado hawajivunii kile walichokifanya na kuahidi kuchukua hatua za kujiimarisha zaidi kwa kuanza kujikosoa sasa na kutathmini kilichotokea. Morocco walikuwa na matumaini ya kufika nusu fainali kwa mara ya pili katika historia. Walifanikiwa kufikia hatua hiyo mara ya kwanza huko Qatar miaka minne iliyopita – lakini pia walitolewa na Ufaransa baada ya kuwafunga 2-0.

Ouahbi ameongeza kuwa anaamini wana mwelekeo mzuri ikiwa wataendelea hivyo, ingawa hilo halimaanishi kwamba hawakutaka kushinda kwenye mechi ya jana. Ameahidi kuendelea kujiimarisha zaidi ili kushinda mataji katika siku za usoni kwa kuwa wanatambua kwamba wanawakilisha zaidi ya nchi moja, kuanzia watu wa Morocco hadi na nchi nyingi kote Asia na Afrika.

Morocco itakuwa mwandaaji mwenza wa michuano ijayo ya Kombe la Dunia kwa kushirikiana na Uhispania na Ureno mwaka wa 2030.

Kocha huyo wa Morocco aidha hakusita kuitakia heri Ufaransa katika hatua zinazofuata, akisema anajua wananuia kutwaa kombe na wana sifa zote za ubingwa.