Maelfu ya mashabiki wa soka nchini Argentina wamefurika mitaani kusherehekea ushindi wa mabingwa hao watetezi wa Kombe la Dunia, baada ya kuichapa England mabao 2-1 na kutinga fainali ya Kombe hilo.
Ushindi huo uliopatikana kupitia bao la ushindi la Lautaro Martinez katika dakika za majeruhi, umeamsha hisia kali kutokana na upinzani wa kihistoria na kisiasa kati ya nchi hizo mbili tangu vita vya Visiwa vya Falkland mwaka 1982.
Licha ya kuwepo kwa madai yasiyo na ushahidi kwenye mitandao ya kijamii kuwa michuano hiyo imepangwa kuibeba Argentina na nahodha wao, Lionel Messi, mashabiki wanasema ni ushindi wa wazi na unaleta faraja kubwa wakati huu taifa hilo likikabiliwa na mgogoro wa kiuchumi.
Argentina sasa itachuana na Uhispania katika mchezo wa fainali uliopangiwa kufanyika Jumapili hii.

