You are currently viewing MOROTO APONGEZA MSAADA WA SERIKALI, ATOA WITO WA AMANI POKOT MAGHARIBI

MOROTO APONGEZA MSAADA WA SERIKALI, ATOA WITO WA AMANI POKOT MAGHARIBI

Mbunge wa Kapenguria katika kaunti ya Pokot Magharibi Samwel Moroto ameipongeza serikali kuu kwa msaada ambao ilitoa kwa shule ya msingi ya Nasokol kufuatia mkasa wa moto ulioteketeza bweni la shule hiyo takriban miezi miwili iliyopita.

Akizungumza alipozuru shule hiyo siku moja tu baada ya maafisa kutoka serikali kuu kutoa msaada huo, Moroto amesema kwamba vifaa hivyo vitasaidia pakubwa katika kuhakikisha kwamba shule hiyo inarejea katika hali yake ya awali kabla ya mkasa huo.

Aidha Moroto amesema kwamba afisi yake itashirikiana kwa karibu na shule hiyo ambayo ni moja ya shule kongwe zaidi katika kaunti ya Pokot Magharibi, katika kuboresha mazingira ya wanafunzi pamoja na walimu kuendeshea shughuli zao za elimu bila ya changamoto.

Kando na hayo Moroto ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wakaazi wa kaunti hiyo kuendelea kudumisha amani hasa kipindi hiki ambapo taifa linakaribia uchaguzi mkuu wa mwaka ujao, akiwataka pia viongozi wa kisiasa kujitenga na siasa za kukoseana heshima.