You are currently viewing SHOLEI NA PUKOSE WAPUUZILIA MBALI MADAI YA KUVURUGWA KWA MFUMO WA UCHAGUZI

SHOLEI NA PUKOSE WAPUUZILIA MBALI MADAI YA KUVURUGWA KWA MFUMO WA UCHAGUZI

Mbunge wa Endebess, Robert Pukose, amekosoa baadhi ya vyombo vya habari nchini kufuatia taarifa zinazodai kumhusisha na usajili wa raia wa uganda kama wapiga kura nchini.

Kwenye kikao cha bunge Pukose amepinga madai hayo na kuvitaka vyombo vya  habari  kuzingatia maadili ya taaluma na kufanya uhakiki wa taarifa kabla ya kuzichapisha vilevile  kuhakikisha habari zinazotolewa zinazingatia maslahi ya umma.

Amesema vyombo vya habari vina wajibu wa kutoa taarifa zilizo sahihi na zilizothibitishwa, hasa katika masuala  yanayoweza kuathiri sifa za watu au kuibua wasiwasi miongoni mwa wananchi.

Kauli hiyo imeungwa mkono na naibu spika wa bunge la kitaifa, Gladys Boss Shollei, ambaye ameonya kuwa madai ya wizi wa kura yanaweza kuchochea machafuko nchini.

Shollei amesema kauli zinazotilia shaka usalama na uadilifu wa mfumo wa uchaguzi zinaweza kudhoofisha imani ya wananchi katika mchakato wa uchaguzi na matokeo yake.

Aidha, Shollei amesisitiza umuhimu wa viongozi na wadau wa uchaguzi kutumia lugha inayolinda imani ya wananchi katika mchakato wa kidemokrasia, huku wakihimiza amani na utulivu kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

APERIT FM,HII NI YETU