Mbunge wa Sigor, Peter Lochakapong, ameibuka kinara wa utendakazi miongoni mwa wabunge wa Kaunti ya Pokot Magharibi, kulingana na utafiti wa hivi punde wa Infotrak.
Matokeo ya utafiti huo yanaonyesha kuwa Lochakapong alipata kiwango cha kuidhinishwa cha asilimia 69, akiongoza orodha ya wabunge wa kaunti hiyo.
Nafasi ya pili inashikiliwa na Mbunge wa Kacheliba Titus Lotee kwa asilimia 62, huku Mbunge wa Kapenguria, Samuel Moroto, akifuatia katika nafasi ya tatu kwa asilimia 61.
Infotrak ilitoa matokeo ya wabunge watatu bora pekee katika kaunti hiyo. Hali hiyo inaashiria kuwa Mbunge wa Pokot South, David Pkosing, hakufanikiwa kuingia katika orodha ya wabunge watatu waliofanya vyema zaidi kwenye tathmini hiyo.
Utafiti wa Infotrak hupima maoni ya wananchi kuhusu utendakazi wa viongozi wao kwa kuzingatia vigezo mbalimbali, ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo, uwajibikaji, upatikanaji wa kiongozi kwa wananchi na kutimiza ahadi za uchaguzi.

