You are currently viewing MCHEZO WA SATARANJI HAPA NCHINI WAPEWA SIFA

MCHEZO WA SATARANJI HAPA NCHINI WAPEWA SIFA

Zaidi ya wanafunzi 800 katika Kaunti ya Trans-Nzoia, wameukumbatia mchezo huo wa sataranji kwa maana ya chess, kama njia moja wapo ya kukabiliana na ongezeko la matumizi ya skrini na urahibu wa mitandao ya kijamii.

Mwenyekiti wa chama cha Sataranji katika kaunti ya Tras-Nzoia Paul Eseme, ameutaja mchezo huo kuwa unao wasaidia wanafunzi kuimarisha umakini, uwezo wa kufikiri kwa kina, kutatua changamoto, kujenga nidhamu, uvumilivu, ujuzi na ustahimilivu.

Eseme pia ameipongeza wizara ya elimu kwa kujumuisha mchezo wa sataranji kuwa miongoni mwa michezo ya ushindani, katika kalenda ya michezo ya muhula wa pili katika shule za umma nchini, akisema kuwa hatua hiyo itasaidia kukuza vipaji, kuongeza ushirika wa wanafunzi na kuimarisha maendeleo ya kiakili na kitaaluma nchini.

Kauli ya Eseme imetiliwa mkazo na walimu Fredrick Odhiambo, Daniel Wekesa wa shule ya upili ya Makunga, na Mnaho Mwende wa shule ya upili ya wasichana ya St. Monica Kitale.

Aidha walimu hao, wamewataka wakuu wa mashule hapa nchini, kukumbatia mchezo huo wa sataranji mashuleni na kuufanya kipaumbele kwa wanafunzi.