You are currently viewing MURGOR ATAKA KUDHIBITIWA KWA SEKTA YA MADINI NCHINI

MURGOR ATAKA KUDHIBITIWA KWA SEKTA YA MADINI NCHINI

Seneta wa Kaunti ya Pokot Magharibi, Julius Murgor, amesema shughuli za uchimbaji haramu wa dhahabu zimesababisha uharibifu mkubwa wa ardhi katika maeneo mbalimbali ya kaunti hiyo, huku akitoa wito kwa serikali kuimarisha sheria na usimamizi wa sekta hiyo.

 Murgor amesema wachimbaji haramu wamekuwa wakielekeza maji ya mito kwenye maeneo ya uchimbaji, jambo ambalo linaathiri mtiririko wa maji na kuhatarisha upatikanaji wa rasilimali hiyo muhimu kwa wananchi na mifumo ya ikolojia.

Aidha ameeleza kuwa baada ya kukamilisha shughuli zao, wachimbaji huacha mashimo makubwa wazi  , hali inayoweka maisha ya wakazi na mifugo katika hatari, pamoja na kuchangia uharibifu wa mazingira.

Murgor ameitaka serikali kuangazia  upya na kuimarisha kanuni zinazosimamia shughuli za uchimbaji wa madini ili kukomesha uchimbaji haramu, kulinda mazingira na kuhakikisha wanaokiuka sheria wanachukuliwa hatua kali.