Gavana wa kaunti ya Elgeyo Marakwet, Wisley Rotich, amewataka wakazi kuchukua tahadhari kufuatia utabiri wa mvua za El Niño ambao unatarajiwa kusababisha changamoto katika maeneo mbalimbali ya kaunti hiyo.
Aidha, gavana Rotich amesema serikali ya kaunti inapanga kuwahamisha kwa lazima wakazi wanaoishi katika maeneo yaliyo katika hatari ya maporomoko ya ardhi.
Amesema hatua hiyo inalenga kuzuia maafa mengine kama yaliyoshuhudiwa katika eneo la Chesongoch, huku serikali ikisisitiza umuhimu wa wakazi kushirikiana na mamlaka wakati wa utekelezaji wa hatua za usalama.
Rotich amewataka wananchi kuwa waangalifu, kufuatilia taarifa za hali ya hewa na kuzingatia maagizo ya serikali ili kulinda maisha na mali zao wakati wa msimu wa mvua.
Aidha amewataka wenyeji kutumia kipindi hicho cha mvua kuzalisha vyakula ili kuondokana na njaa hasa baada ya kipindi kirefu cha kiangazi kilichosababisha hasara msimu huu
APERIT FM,HII NI YETU

