Mgombea wa kiti cha uwakilishi wa akina mama katika Kaunti ya Baringo, Dkt. Rebecca Lomong, ametoa wito kwa jamii za wafugaji katika eneo la North Rift kuweka kipaumbele elimu ya mtoto wa kike ili kuongeza nafasi za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Akizungumza kwa lugha ya kalenjin Dkt. Lomong amesema elimu ndiyo msingi wa kuwawezesha wasichana kufikia ndoto zao, kujitegemea na kuchangia maendeleo ya familia na jamii kwa ujumla.
Amesisitiza kuwa kuwapa wasichana nafasi ya kupata elimu bora ni uwekezaji wa muda mrefu unaonufaisha kizazi cha sasa na kijacho.
Aidha, amewataka wazazi na viongozi wa jamii kushirikiana katika kupambana na changamoto zinazowazuia wasichana kuendelea na masomo, ikiwemo ndoa za utotoni, mimba za mapema na mila zinazokatiza elimu yao.
Dkt. Lomong ameeleza kuwa jamii itakapowekeza katika elimu ya mtoto wa kike, itaongeza idadi ya wanawake wenye ujuzi na taaluma mbalimbali, jambo litakalosaidia kupunguza umaskini na kuimarisha maendeleo katika eneo la North Rift.

