You are currently viewing RAIS RUTO ASISITIZA MAGEUZI KATIKA BARAZA LA USALAMA LA UMOJA WA MATAIFA

RAIS RUTO ASISITIZA MAGEUZI KATIKA BARAZA LA USALAMA LA UMOJA WA MATAIFA

 Rais William Ruto ameitaka jumuiya ya kimataifa kufanya mageuzi katika baraza la usalama la umoja wa mataifa, akisema mfumo wa sasa hautoi uwakilishi sawa kwa mataifa yote.

Akizungumza katika mkutano mkuu wa 81 wa umoja wa mataifa mjini New York, amelalamikia hali kwamba afrika, yenye nchi 54 wanachama wa umoja wa mataifa, bado haina uwakilishi wa kudumu katika baraza la usalama licha ya bara hilo kuathiriwa mara kwa mara na maamuzi ya baraza hilo kuhusu amani na usalama.

Rais Ruto amesema hali hiyo inaonyesha pengo kati ya usawa unaotambuliwa katika baraza kuu la umoja wa mataifa na mgawanyo wa mamlaka ndani ya baraza la usalama.

Kiongozi wa taifa  Ruto  amekosoa kile alichokitaja kuwa matumizi yasiyolingana ya sheria za kimataifa, akisema imani katika mfumo wa kimataifa haiwezi kurejeshwa iwapo sheria zitatumiwa kwa viwango tofauti katika migogoro mbalimbali.

Amesema mageuzi ya taasisi za kimataifa  ni  muhimu  katika  kurejesha imani na kuhakikisha mataifa yote yanakuwa na sauti katika maamuzi yanayohusu mustakabali wao.

Rais amesema mageuzi hayo yanapaswa kulenga kujenga umoja wa mataifa ambao kila taifa lina sauti, kila taifa lina nafasi ya kushiriki na kila kizazi kinaweza kutegemea mfumo wa kimataifa unaozingatia usawa na uwajibikaji.

APERIT FM,HII NI YETU