Mbunge wa Nandi Hills, Bernard Kitur, amewahimiza wakazi wa kaunti ya Nandi kuwachagua viongozi wanaotekeleza majukumu yao kwa ufanisi katika uchaguzi ujao.
Amesema kuwa kuwarejesha viongozi hao madarakani kutahakikisha miradi ya maendeleo iliyoanzishwa inakamilika kwa wakati na wananchi wanaendelea kunufaika na huduma bora.
Kitur amesema maendeleo ya kweli yanahitaji mwendelezo wa uongozi na utekelezaji wa mipango ya muda mrefu, akieleza kuwa kubadilisha viongozi mara kwa mara kunaweza kuchelewesha utekelezaji wa miradi muhimu na kuathiri kasi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali.
Amebainisha kuwa sekta kama elimu, afya, miundombinu ya barabara, maji na kilimo zinahitaji sera na uongozi thabiti ili ziweze kuleta matokeo yanayokusudiwa, akitoa wito kwa wananchi kutathmini viongozi kwa kuzingatia rekodi ya utendaji wao badala ya misingi mingine wakati wa kufanya maamuzi ya uchaguzi.

