Mbunge wa Kesses, CPA Julius Rutto, amesema Kamati ya Bunge ya Fedha na Mipango ya Kitaifa, ambayo yeye ni mwanachama, itachunguza kwa kina ucheleweshaji wa muda mrefu wa malipo ya pensheni na mafao ya wastaafu wanaowemo walimu pamoja na watumishi wengine wa umma.
Akizungumza kuhusu suala hilo, Mbunge huyo amesema kucheleweshwa kwa mafao ya wastaafu kumeendelea kuwa changamoto inayowaathiri maelfu ya waliolitumikia taifa kwa miaka mingi. Amesisitiza kuwa ni haki ya wastaafu kupokea malipo yao kwa wakati ili waweze kuendesha maisha yao bila matatizo ya kifedha.
Aidha Rutto amebainisha kuwa kamati hiyo itashirikiana na Wizara ya Fedha pamoja na idara husika kubaini sababu za ucheleweshaji huo na kupendekeza hatua za kudumu za kuhakikisha pensheni na mafao ya kustaafu yanatolewa kwa wakati.
wakati huo uo amewahakikishia walimu wastaafu na watumishi wengine wa umma kuwa Bunge lina dhamira ya kulinda maslahi yao na kuhakikisha mifumo ya malipo inaimarishwa ili kuondoa ucheleweshaji unaowasababishia mateso baada ya kumaliza utumishi wao.

